TAEC: TANZANIA YALENGA KUANZA KUZALISHA UMEME WA NYUKLIA NDANI YA MIAKA SABA
DAR ES SALAAM – Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) imesema Serikali imeweka lengo la kuanza kuzalisha umeme wa nyuklia ndani ya takribani miaka saba ijayo, huku ikiendelea na maandalizi ya kutimiza viwango vya usalama vinavyotakiwa kimataifa.
Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Prof. Najat K. Mohammed, amesema hayo katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, ambapo amewakaribisha wananchi kutembelea banda la TAEC lililopo ndani ya Jumba la China ili kujifunza matumizi ya teknolojia ya nyuklia.
Prof. Najat amesema teknolojia ya nyuklia ina matumizi mengi katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, afya, viwanda na ujenzi. Amesema katika kilimo hutumika kuboresha mbegu na kuongeza uzalishaji wa maziwa, huku sekta ya afya ikinufaika kupitia uchunguzi na matibabu ya magonjwa kama saratani.
Amesema matumizi makubwa zaidi yanayolengwa kwa sasa ni uzalishaji wa umeme wa nyuklia, ambao una faida ya kuzalisha umeme kwa muda wote bila kukatika na bila kutoa hewa ya ukaa inayochangia mabadiliko ya tabianchi.
"Umeme wa nyuklia ni umeme kama umeme mwingine tunaoutumia majumbani, tofauti yake ni chanzo chake. Nishati hutokana na mpasuko wa nyuklia unaozalisha nguvu kubwa inayotumika kuzalisha umeme wa uhakika na rafiki kwa mazingira," amesema.
Prof. Najat amesema TAEC inaendelea na maandalizi ya kutekeleza mradi huo kwa kufuata viwango vya usalama vya kimataifa vinavyosimamiwa na International Atomic Energy Agency (IAEA). Amesema wataalamu wa wakala huo wanatarajiwa kuja nchini kufanya tathmini ya utayari wa Tanzania kuingia katika hatua ya kwanza ya utekelezaji wa mpango wa umeme wa nyuklia.
Ameeleza kuwa hatua hiyo itajumuisha kuimarisha mfumo wa sheria, kanuni na taasisi za usimamizi ili kuhakikisha usalama wa wananchi na mazingira katika matumizi ya teknolojia ya nyuklia.
Kuhusu malighafi, Prof. Najat amesema Tanzania ina akiba ya madini ya urani, ambayo ndiyo malighafi ya kuzalisha umeme wa nyuklia, huku mradi wa Mkuju River uliopo mkoani Ruvuma ukiwa miongoni mwa maeneo yaliyofikia hatua za maandalizi ya uchimbaji.
Amesema urani inayochimbwa nchini italazimika kufanyiwa uchakataji maalumu kabla ya kutumika kama mafuta ya kuzalisha umeme wa nyuklia, huku akisisitiza kuwa wananchi wasiogope teknolojia hiyo kwa kuwa matumizi yake ya amani ni salama yanapozingatia viwango vya kimataifa.
Prof. Najat amesisitiza kuwa nyuklia si sawa na mabomu ya nyuklia, akieleza kuwa teknolojia hiyo ina matumizi mengi ya maendeleo yanayochangia ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii inapodhibitiwa kwa kufuata taratibu za usalama.




