MUHITIMU ASIYEONA WA VETA TANGA AVUNJA VIKWAZO, AANGAZIA UJUZI WA USEREMALA
Dar es Salaam: Ernest Mashiku Igobeko, mwenye ulemavu wa kutoona kabisa na mhitimu wa kozi fupi ya useremala katika Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Tanga, amesema ulemavu haupaswi kuwa kikwazo cha kupata ujuzi na kujitegemea.
Akizungumza wakati wa maonesho, Ernest alisema baada ya kuhitimu mafunzo alikumbana na changamoto ya kupata sehemu ya kufanya mazoezi kwa vitendo, huku baadhi ya mafundi wakikataa kumpokea kutokana na hali yake. Hata hivyo, alisema baadaye alipata fundi aliyemkubali na kumpa nafasi ya kuendelea kujifunza kwa vitendo.
Alieleza kuwa kupitia mafunzo hayo amejifunza aina mbalimbali za viungo vya useremala vinavyotumika kuunganisha mbao, ikiwemo mortise and tenon, mitre joint, rebated joint, tongue and groove, plain butt joint pamoja na viungo vingine vinavyotumika kutengeneza meza, viti, makabati na bidhaa nyingine za samani.
Ernest alisema mafunzo hayo pia yanajumuisha mbinu za kuongeza upana wa mbao, kuunganisha mbao kwa usahihi na kutengeneza bidhaa imara zinazodumu kwa muda mrefu.
Aidha, alisema wamefundishwa kutengeneza aina mbalimbali za milango, ikiwemo milango ya aluminium na ya mbao, kwa kujifunza hatua zote kuanzia kukata malighafi, kuunganisha sehemu mbalimbali hadi kukamilisha bidhaa.
Alibainisha kuwa ujuzi alioupata unamwezesha kufanya kazi za useremala kama fundi mwingine yeyote, na kutoa wito kwa waajiri na jamii kutowabagua watu wenye ulemavu bali kuwapa fursa ya kuonesha uwezo wao kupitia ujuzi walioupata.




