Breaking News

TANESCO YATOA ELIMU YA TEKNOLOJIA YA NYUMBA JANJA SABASABA

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetoa elimu kwa wananchi kuhusu teknolojia ya Nyumba Janja (Smart House), inayomwezesha mtumiaji kudhibiti vifaa vya umeme akiwa popote alipo kupitia simu ya mkononi.

Akizungumza Julai 4, 2026 katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO, Irine Gowelle, amesema mfumo huo unatumia programu ya Smart Life, inayomwezesha mtumiaji kuwasha na kuzima vifaa vya umeme kwa njia ya mtandao hata akiwa mbali na nyumba yake.

Amesema teknolojia hiyo pia humwezesha mtumiaji kufuatilia matumizi ya umeme ya kila siku, kubaini kifaa kinachotumia umeme mwingi na hivyo kupanga matumizi bora ya nishati kwa ufanisi.

"Mtumiaji anaweza kupanga muda wa kuwasha na kuzima vifaa vya umeme pamoja na kudhibiti matumizi ya soketi na swichi za umeme popote alipo, mradi awe na huduma ya intaneti," amesema Gowelle.

Aidha, amesema mfumo huo hutoa taarifa za hitilafu zinazoweza kujitokeza kwenye vifaa vya umeme vilivyounganishwa, kupitia simu ya mkononi, jambo linalomwezesha mtumiaji kuchukua hatua kwa wakati na kuongeza usalama wa matumizi ya umeme.

TANESCO imesema utoaji wa elimu hiyo unalenga kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika usimamizi wa nishati na kuunga mkono safari ya taifa kuelekea uchumi wa kidijitali.