Breaking News

JWTZ YAONYA DHIDI YA UCHOCHEZI, YASISITIZA HATUA KALI KWA WAVUNJIFU WA AMANI

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limesema litachukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu yeyote atakayejihusisha na vitendo vinavyohamasisha vurugu, ghasia na uvunjifu wa amani nchini.

Katika taarifa yake kwa umma, JWTZ imeeleza kuwa jukumu lake la kulinda usalama wa nchi na wananchi linatokana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na Sheria ya Ulinzi wa Taifa, Sura ya 192.

Jeshi hilo limesisitiza kuwa litaendelea kushirikiana na vyombo vya dola kuhakikisha linakabiliana kwa ufanisi na matukio yoyote yanayoweza kuhatarisha amani na usalama wa taifa.

Vilevile, JWTZ limewataka wananchi kushiriki katika kulinda amani kwa kutoa taarifa kwa viongozi wa vijiji, mitaa pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kuhusu viashiria vyovyote vya uchochezi au vitendo vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa nchi.

Aidha, jeshi hilo limewahakikishia wananchi kuwa litaendelea kutekeleza wajibu wake wa kulinda mipaka ya nchi, Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku likiendelea kushirikiana na wananchi katika kuimarisha amani, umoja na maendeleo ya taifa.