TTCL YAJIVUNIA FAIDA YA BILIONI 23, YAONGEZA UBUNIFU NA KASI YA UCHUMI WA KIDIJITALI
Dar ea salaam - Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limesema limeendelea kuimarisha huduma za mawasiliano ya kidijitali nchini kupitia matumizi ya Mkongo wa Taifa, huku likitangaza kupata faida ya takribani Sh bilioni 23 katika mwaka wa fedha 2024/25.
Akizungumza katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, alisema shirika hilo limejikita katika kuunga mkono utekelezaji wa uchumi wa kidijitali kwa kutoa huduma za intaneti zenye kasi, ubora na gharama nafuu.
Alisema TTCL linatumia Mkongo wa Taifa unaomilikiwa na kuendeshwa na shirika hilo kuhakikisha Watanzania wanapata huduma za mawasiliano zinazokidhi mahitaji ya uchumi wa kisasa.
Marwa alisema miongoni mwa huduma mpya zilizoletwa mwaka huu ni SuperNIX Speed, huduma ya intaneti yenye kasi kubwa ambayo, kwa mujibu wa shirika hilo, inatoa viwango vya juu vya kasi kuliko huduma zinazotolewa na waendeshaji wengine wa mitandao ya simu na watoa huduma za intaneti nchini.
Aidha, alisema TTCL limezindua FTTx Experience Center, kituo kinachoonesha matumizi ya intaneti katika kuendesha nyumba janja (Smart Home), ikiwemo kudhibiti vifaa vya nyumbani kama friji, jiko, mashine za kufulia, mifumo ya ulinzi, pamoja na huduma za burudani kwa kutumia intaneti.
"Teknolojia hizi haziwezi kufanya kazi ipasavyo bila kuwa na intaneti yenye kasi na ubora wa kutosha, ndiyo maana tunaendelea kuwekeza katika huduma zinazotumia Mkongo wa Taifa," alisema.
Marwa pia alisema TTCL limepanua huduma zinazotolewa katika Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data (National ICT Data Centre – NIDC), kwa kuongeza huduma za Cloud Computing, zitakazowawezesha wateja kuhifadhi taarifa zao bila kulazimika kuwekeza katika miundombinu mikubwa ya kuhifadhi data.
Alieleza kuwa hatua hiyo itawasaidia taasisi, kampuni na wafanyabiashara kupunguza gharama za uwekezaji huku wakinufaika na huduma salama za uhifadhi wa taarifa.
Kuhusu utendaji wa shirika, Marwa alisema mafanikio ya kupata faida yanatokana na maboresho yaliyofanyika katika uendeshaji wa TTCL kufuatia maelekezo ya Rais ya kuendesha shirika kibiashara na kwa tija.
Alisema kwa mwaka wa fedha 2024/25 TTCL limepata faida ya takribani Sh bilioni 23, huku akibainisha kuwa matokeo ya awali ya mwaka wa fedha 2025/26 yanaonesha ongezeko la mapato na matarajio ya faida kubwa zaidi, ingawa takwimu rasmi zitatolewa baada ya kukaguliwa.
"Tunaamini kipindi cha TTCL kupata hasara kimekwisha. Sasa tunaendelea kukuza mapato, kuongeza idadi ya wateja na kuendesha shirika kwa ufanisi huku tukizalisha faida," alisema.




