WANNE WAJITOKEZA KUONGOZA NGOME YA VIJANA ACT WAZALENDO
Makada Wanne wa ACT Wazalendo wametangaza nia ya kugombea nafasi ya Uenyekiti wa Ngome ya Vijana katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Februari 2024.
Makada hao ni Waziri Kivuli wa Vijana, Kazi na Ajira na Mwenyekiti anayemaliza muda wake Ndugu Abdul Nondo, Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ndolezi Petro, Naibu Waziri Kivuli wa Afya Ruqayya Nassir na Naibu Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara Julius Masabo.
Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma Ndugu Janeth Rithe, uchaguzi wa Viongozi wa Kitaifa wa Ngome za Chama utafanyika kuanzia tarehe 29 Februari. Machi 1; Ngome ya Vijana, Machi 2; Ngome ya Wazee na Machi 3; Ngome ya Wanawake. Mkutano Mkuu wa Kuwachagua Viongozi Wakuu wa Chama (Kiongozi wa Chama, Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wa Halmashauri Kuu) utafanyika tarehe 5-6 Machi 2024.
Ndugu Rithe amesema kwa mujibu wa taratibu za ACT Wazalendo Wanachama wanaruhusiwa kutangaza nia ya kugombea nafasi yoyote wanayoitaka ilimradi wazingatie matakwa ya Katiba na Kanuni za Chama ikiwemo kutoanza kampeni kabla ya wakati.
Imetolewa na Idara ya Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma ACT Wazalendo.
Feb 09, 2024




