Breaking News

MSAJILI WA VYAMA: VYOMBO VYA HABARI VIHESHIMU NA KUFUATA WELEDI KATIKA KUREPOTI UCHAGUZI MKUU

Dar es Salaam – Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, amevitaka vyombo vya habari nchini kuzingatia weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari katika kuripoti matukio ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) uliofanyika katika Ukumbi wa Multifunctional, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Jaji Mutungi alisema kuwa ni wajibu wa vyombo vya habari kuwa vinara katika kuelimisha umma kwa kutoa taarifa sahihi, za ukweli na zisizo na upendeleo.
Ameonya dhidi ya matumizi mabaya ya teknolojia, ikiwemo matumizi ya akili mnemba (AI), katika kusambaza taarifa za upotoshaji, propaganda na uzushi, akisisitiza kuwa hatua hiyo inaweza kuhatarisha amani na usalama wa nchi wakati wa uchaguzi.

Mkutano huo umehusisha vyama vya siasa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), pamoja na TBC, ambapo wadau walijadili nafasi na wajibu wa vyombo vya habari katika uchaguzi mkuu wa 2025 kwa mujibu wa sheria za uchaguzi.

Pamoja na hilo, mkutano huo pia umeangazia uhuru wa Tume ya Uchaguzi katika kuandaa uchaguzi, pamoja na kupokea mapendekezo kutoka kwa wadau kuhusu namna bora ya kuendesha kampeni kwa haki na amani.










Picha zote na tbc digital