JESHI LA POLISI: HALI YA USALAAMA NCHINI NI SHWARI, LATOA ONYO DHIDI YA WANAOHAMASISHA VURUGU
Jeshi la Polisi Tanzania limesemalll hali ya usalama nchini inaendelea kuwa shwari kutokana na ushirikiano uliopo kati ya wananchi, wadau mbalimbali pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama katika kulinda amani na utulivu.
Akizungumza leo Julai 5, 2026, Msemaji wa Jeshi la Polisi, DCP David Misime, amesema taarifa hiyo ni mwendelezo wa taarifa iliyotolewa Juni 19, 2026 kuhusu hali ya usalama nchini.
Amesema pamoja na hali hiyo kuwa tulivu, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama linaendelea kufuatilia kwa karibu viashiria vinavyoonesha kuwa kuna baadhi ya watu wachache wanaodaiwa kupanga kuvuruga amani kwa kutumia visingizio vya kufanya maandamano yasiyofuata taratibu za kisheria na kiusalama.
Kwa mujibu wa Misime, baadhi ya watu hao tayari wamekamatwa na uchunguzi unaendelea ili hatua nyingine za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Aidha, amesema uchunguzi umebaini kuwepo kwa taarifa za uhamasishaji wa vitendo vya vurugu kupitia mitandao ya kijamii na majukwaa ya mijadala mtandaoni, ikiwemo madai ya mipango ya kushambulia viongozi, wananchi, askari wa vyombo vya ulinzi na usalama, kuchoma moto shule pamoja na kuharibu na kupora mali za umma na binafsi.
Jeshi la Polisi limesema vitendo hivyo ni viashiria vinavyotishia usalama wa taifa na haviwezi kuvumiliwa kwa kuwa ni kinyume cha sheria.
Kutokana na hali hiyo, Jeshi limetoa onyo kali kwa mtu au kikundi chochote kitakachojihusisha na vitendo vya uhalifu au kuhamasisha vurugu kupitia mitandao ya kijamii au njia nyingine, likisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika.
Vilevile, Jeshi limewataka wananchi kujiepusha na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa mapema wanapoona viashiria vya uvunjifu wa amani au sheria.
Misime amesema ulinzi umeimarishwa katika maeneo mbalimbali nchini, hususan kuelekea maadhimisho ya Sikukuu ya Sabasaba na Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam.
Amehitimisha kwa kuwahakikishia wananchi kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuhakikisha amani, utulivu na usalama vinaendelea kutawala nchini, huku akiwahimiza wananchi kuendelea na shughuli zao za kila siku bila hofu.




